Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

TFC YATAKIWA KUWA NA MPANGO WA MATUMIZI SAHIHI YA MBOLEA

Imewekwa: 03 Apr, 2025
TFC YATAKIWA KUWA NA MPANGO WA MATUMIZI SAHIHI YA MBOLEA

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, (anayesimamia Ushirika na Umwagiliaji), Dkt. Stephen Nindi ameishauri Menejiment ya Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) kuwa na mpango wa matumizi sahihi ya mbolea ili kuongeza uzalishaji wa mazao bila kuathiri mazingira.

Dkt. Nindi amesema hayo wakati wa kikao chake na timu ya Menejimenti ya Kampuni ya Mbolea Tanzania(TFC) tarehe 28 Machi 2025, jijini Dar es Salaam.

Ameeleza kuwa utumiaji wa mbolea kwa kuzingatia afya ya udongo, mahitaji ya mimea ya eneo husika, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wakulima kutawezesha kuongeza uzalishaji wa mazao.

“Nchi ni kubwa, inahitaji mbolea, lakini tunahitaji matumizi sahihi ya utumiaji wa mbolea kulingana na aina ya mazao/mimea,” ameeleza Dkt. Nindi.

Ameongeza kuwa kufanya utafiti ni muhimu ili kubaini aina ya virutubisho vilivyopo katika udongo na hivyo kutoa mapendekezo kwa wakulima ya aina na kiasi cha mbolea kinachohitajika katika zao husika.

Dkt. Nindi amewataka wataalam wa masoko wa TFC kufanya utafiti wa soko la mbolea kwa kuangalia mafanikio ya wafanyabiashara wengine wanaofanya vizuri kwenye tasnia ya mbolea ili kuongeza ufanisi katika soko la mbolea.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), Bw. Samuel Mshote ameeleza kuwa TFC imeendelea kukua katika biashara ya mbolea kwa kuzingatia malengo ya Serikali kupitia Wizara ya Kilimo.  Bw. Mshote ameongeza zaidi kuwa timu yake itaendelea kuwa wabunifu ili kujifunza zaidi soko na mahitaji ya mbolea kwa wakulima ili kuleta tija zaidi katika Sekta ya Kilimo.