Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

UPIMAJI WA AFYA YA UDONGO ITAONGEZA TIJA YA UZALISHAJI WA MAZAO NCHINI- DC MWENDA

Imewekwa: 11 Nov, 2024
UPIMAJI WA AFYA YA UDONGO ITAONGEZA TIJA YA UZALISHAJI WA MAZAO NCHINI- DC MWENDA
Zoezi la upimaji wa afya ya udongo katika Halmashauri ya Wilaya ya Iramba itasaidia kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao ya kilimo ikiwemo chakula, biashara pamoja na mazao ya bustani. Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Mhe. Suleiman Yusuph Mwenda alipokutana na Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi na Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Kilimo, Eng. Juma Omary Mdeke pamoja na wadau wa kilimo kutoka shirika la Helvetas kwenye Mradi wa UKIJANI wakati wa ufuatiliaji wa zoezi la upimaji wa afya ya udongo linaloendela Wilayani humo kuanzia tarehe 4 Novemba 2024. “Zoezi hili la upimaji wa afya udongo litatusaidia kutambua aina ya udongo, mazao yapi yanafaa kulimwa katika eneo husika na kupata matumizi sahihi ya mbolea,” amesema Mhe. Mwenda. Naye Eng. Juma Omary Mdeke amesema zoezi hilo litahusisha vijiji  78 katika Halmashauri hiyo  na kuchukua Sampuli zisizopungua 400 kwa ajili ya uchakataji na kupata matokeo sahihi na kuwaelimisha wakulima namna gani ya kulima ili kufikia malengo ya Serikali kupitia Agenda 10/30. Aidha, kwa upande wake Meneja wa Mradi wa UKIJANI kutoka shirika la Helvetas Mkoani Singida, Bi. Shoma Nangale ameipongeza Wizara ya Kilimo kwa mpango huo madhubuti wa upimaji wa afya ya udongo ambao  utasadia kukuza uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa kuwa Udongo ndio chanzo cha kilimo. Baada ya Kukamilisha ufuatiliaji wa zoezi hilo la upimaji wa afya ya udongo Wilayanii Iramba, Eng. Mdeke aliambata na Meneja wa Mradi wa UKIJANI, Bi. Shoma Nangale kutoka Shirika la Helvetas kutembelea maeneo mbalimbali ya wanufaika wa mradi huo katika wilaya ya Ikungi pamoja na Wilaya ya Manyoni Mkoani Singida tarehe 4-5 Novemba, 2024. Wizara ya Kilimo imeendelea kuhamasisha matumizi endelevu ya ardhi ya kilimo kwa kutekeleza zoezi la kutambua na kupima afya ya udongo kwa nchi nzima  ili kuandaa ramani ya udongo nchi nzima itakayo onesha hali ya udongo ili kuongeza tija na uzalishaji ili kufikia lengo la kukuza Sekta ya Kilimo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.