Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

USIMAMIZI WA BIASHARA YA MAZAO NI KWA MANUFAA YA WAKULIMA NA WAFANYABIASHARA

Imewekwa: 11 Nov, 2024
USIMAMIZI WA BIASHARA YA MAZAO NI KWA MANUFAA YA WAKULIMA NA WAFANYABIASHARA
Serikali imeanzisha mifumo na taratibu za usimamizi wa biashara za mazao ya nafaka na mchanganyiko ili kuwezesha upatikanaji wa  faida zenye maslahi kwa wakulima na wafanyabiashara. Hayo yamesemwa na  Afisa  Kilimo Mkuu wa  Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao mchanganyiko (COPRA) Bi. Mary Majule katika viwanja vya maonesho ya kuelekea kilele cha siku ya chakula duniani yanayofanyika kwenye viwanja vya CCM manispaa ya Bukoba mkoani Kagera. Akitoa mfano wa utaratibu wa stakabahi za ghala na mfumo wa minada ya kidijitali kupitia Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) kwenye mazao ya ufuta, dengu, mbaazi, soya na kakao, Bi. Majule amesema nia ya serikali ni kulinda maslahi ya wakulima na wafanyabiashara wa mazao hayo. Aidha Bi. Majule amebainisha kuwa mfumo huo utawezesha upatikanaji wa takwimu za kibiashara ikiwa ni pamoja na masoko, bei na takwimu za uzalishaji na usafirishaji.  Bi. Majule ameongeza kuwa utaratibu wa minada ya kidijitali utaongeza uwazi kati ya mkulima na mfanyabiashara ambapo kila mmoja atauza na kununua kwa bei itayozingatia maslahi na hatimaye kuboresha maisha ya mkulima na mfanyabiashara. Bi. Majule amewakaribisha wananchi wote kutembelea banda la COPRA kwenye maonesho ya kuelekea siku ya chakula duniani yanayofanyika kwenye viwanja vya CCM Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera ili wapate elimu zaidi.