WADAU TASNIA YA PARACHICHI WAJITOKEZA KWA WINGI KATIKA MKUTANO WA KWANZA KITAIFA WA ZAO HILO

Wadau mbalimbali wa Tasnia ya Parachichi nchini wamejitokeza kwa wingi katika Mkutano wa Kwanza wa Kitaifa wa zao hilo tarehe 4 Aprili 2025, jijini Dodoma ambao Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli aliufungua na kuwahasa wadau kutumia jukwaa hilo kama nyenzo ya kuimarisha mifumo ya uzalishaji na uendeshaji wa zao hilo.
Wadau hao waliojitokeza kwa mamia ni pamoja na Wakulima wa Parachichi, Wanunuzi na Wasafirishaji, Wakuu wa Mikoa inayozalisha Parachichi ambayo ni pamoja na Njombe, Mbeya, Kigoma, Songwe na mengine; Waheshimiwa Wabunge, Wadau wa Maendeleo na Sekta Binafsi.
Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) imeratibu Mkutano huo chini ya Mkurugenzi Mkuu, Bi. Irene Mlola ambaye amewaeleza washiriki wa Mkutano huo kuwa unaashiria dhamira ya Wizara ya Kilimo kuwa na Mamlaka hiyo kama kiungo cha kuendelea kuwa sikivu kwa wadau wa zao hilo katika kutatua changamoto zao; ikiwa ni pamoja na za wakulima wa mazao mengine yanayoratibiwa chini ya usimamizi wa Mamlaka hiyo.