WAJUMBE BENKI YA DUNIA WAKOSHWA NA UTEKELEZAJI WA PROGRAMU YA TFSRP

Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na wajumbe wa Benki ya Dunia (WB) wakiongozwa na Bi. Frauke Jungbluth ambaye ni Meneja Kilimo na Chakula katika ukanda wa Kusini na Mashariki ya Afrika wa Benki ya Dunia (Practice Manager Agriculture and Food in Southern and Eastern Africa World Bank) tarehe 11 Machi 2025 katika ofisi za Wizara, jijini Dodoma.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu (anayeshughulikia Ushirika na Umwagiliaji), Dkt. Stephen J. Nindi, Mratibu wa Programu ya Mifumo Himilivu ya Chakula Tanzania (TFSRP), Bw. Timothy Semuguruka pamoja na wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo.
Aidha, Wajumbe kutoka Benki ya Dunia (WB) wapo katika ziara ya kutembelea Wizara ya Kilimo kuanzia tarehe 10 hadi 14 Machi 2025. Ziara hiyo imelenga kuangalia utekelezaji wa Programu ya Mifumo Himilivu ya Chakula Tanzania (TFSRP) ambapo wajumbe hao wameipongeza Wizara kwa kutekeleza programu hiyo kwa ufasaha na kushauri watekelezaji wa programu kuwa na matokeo chanya kwa ajili ya kufanya mageuzi zaidi katika Sekta ya Kilimo.
Wajumbe kutoka Benki ya Dunia (WB) wanaendelea na ziara jijini Dodoma katika Taasisi za Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NiRC) na Kiwanda cha ITRACOM na kutarajia kuihitimisha ziara yao Zanzibar tarehe 14 Machi 2025.