WAKULIMA WATAKIWA KUWA NA ELIMU YA MBEGU BORA
WAKULIMA WATAKIWA KUWA NA ELIMU YA MBEGU BORA
Imewekwa: 11 Nov, 2024
Elimu ya matumizi na utambuzi wa mbegu zilizothibitishwa ubora na Mamlaka ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI ) ni maarifa muhimu kwa mkulima ili aweze kupata matokeo mazuri shambani na kuepuka hasara zinazosababishwa na upandaji wa mbegu zisizo na ubora.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kanda ya Ziwa wa Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) Bw. Ayubu Mushema alipozungumza na wananchi waliofika kwenye banda la TOSCI kwenye Maadhimisho ya kuelekea kilele cha Siku ya Chakula Duniani yanayofanyika kwenye viwanja vya CCM Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.
Bw. Mushema amebainisha kuwa baadhi ya wakulima wamekuwa wakipata hasara baada ya kununua na kupanda mbegu zisizo na ubora ambazo zimekuwa zikitoa mavuno hafifu na kupelekea hasara ya kifedha kwa wakulima.
Bw. Mushema alisema kuwa mkulima anaponunua mbegu ni lazima ajiridhishe kama kifungashio cha mbegu kimetaja jina la mzalishaji, aina ya zao, aina ya mbegu, daraja la mbegu, namba ya fungu (lot number), kiwango cha usafi (%), kiwango cha uotaji (%), tarehe ya kupimwa ubora kwenye maabara na matumizi ya lebo za TOSCI .
Aidha, Bw. Mushema amewakaribisha wananchi wote wa mkoa wa kagera kufika kwenye maonesho ya kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani ili wapate maarifa zaidi yatakayowawezesha kuepuka hasara zinazotokana na matumizi ya mbegu zisizo na ubora.
Maonesho ya maadhumisho ya Siku ya Chakula Duniani yameanza tarehe 10 Oktoba, 2024 na kilele chake itakuwa tarehe 16 Oktoba, 2024.