WAZIRI BASHE AITAKA NIRC KUSHIRIKIANA NA WAKURUGENZI WA HALMASHAURI KATIKA UTEKELEZAJI NA UENDESHAJI WA MIRADI YA UMWAGILIAJI

Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) ameitaka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) kushirikiana na Wakurugenzi wa Halmashauri katika kusimamia na kutekeleza miradi ya umwagiliaji nchini katika kuhakikisha inakua endelevu kwa shughuli za kilimo.
Waziri Bashe ameyasema hayo katika Hafla ya Utiaji Saini Makubaliano na Wakurugenzi wa Halmashauri 19 nchini juu ya Usimamizi na Uendeshaji wa Matunzo ya Skimu za Umwagiliaji, kati ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na Vyama vya Umwagiliaji kupitia mradi wa Mifumo Himilivu ya Chakula (TFSRP), tarehe 24 Januari 2025 jijini Dodoma.
Makubaliano hayo yanahusisha usimamizi wa skimu 23 zinazokarabatiwa kwa mkopo wa masharti nafuu kupitia mradi wa TFSRP, aidha katika utekelezaji wa mradi huo Tume imenunua magari 17 pamoja na mitambo kwa ajili ya uchimbaji wa visima 56,000 lengo likiwa ni kukiwezesha kisima kimoja kumwagilia hekari 40 za mashamba ya wakulima.
Mradi wa TFSRP unagharimu Dola za Marekani Milioni 300 ambapo kati ya hizo Tume ya Umwagiliaji imepata jumla ya Dola za Marekani Milioni 70, ikilenga kuchimba visima 67,000, kuongeza eneo la umwagiliaji kufikia hekta 37,000, ununuzi wa mitambo 15 ya uchimbaji wa visima pamoja na ujenzi wa skimu za umwagiliaji.
Hafla hiyo imehusisha Wakurugenzi wa Halmashauri ya Morogoro vijijini, Ifakara, Kongwa, Dodoma jiji, Mufindi, Kilolo, Iringa mji, Mbarari, Nzega, Korogwe, Lushoto, Moshi mji, Meru, Sikonge, Igunga, Kilosa ,Same, Hai pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mwanga.