Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

Waziri Bashe atoa maelekezo kwa TOSCI na TFRA kuunda jukwaa la Wafanyabiashara wa Pembejeo

Imewekwa: 18 Dec, 2024
Waziri Bashe atoa maelekezo kwa TOSCI na TFRA kuunda jukwaa la Wafanyabiashara wa Pembejeo

Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) ametoa maelekezo kwa Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) na Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) kukaa pamoja na kuunda jukwaa la wafanyabiashara wa pembejeo ambalo litakuwa na matawi matatu ya kusemea masuala ya mbolea, viuatilifu na mbegu.

Amesema kuwa matawi hayo yataiwezesha Serikali kuwa na majadiliano na tasnia husika katika kukabiliana na changamoto zozote ili kuondoa kero kwa wakulima na wafanyabiashara.  Mhe. Bashe ameongea hayo tarehe 17 Desemba 2024 jijini Dodoma wakati wa kikao chake na wadau wa tasnia ya mbegu nchini wakiwemo Chama cha Wafanyabiashara wa Mbegu, Wazalishaji, Makampuni na Mawakala wa Mbegu.

Waziri Bashe pia ametoa wito kwa wazalishaji wa mbegu kuruhusu ‘agro-dealers’ wanaowaamini kununua mbegu moja kwa moja katika vituo vikuu vya usambazaji (depot) kwa bei ya ruzuku kwa ajili ya kumnufaisha mkulima mlengwa.  

“Tuondokane na utumiaji wa njia zisizo rasmi.  Ruzuku ni kichocheo cha kusaidia wakulima kuzalisha kwa bei nafuu lakini pia kurasimisha usajili wa wakulima na wafanyabiashara ambao kama wanufaika,” amesema Mhe. Waziri Bashe. 

Mhe. Waziri Bashe amebainisha kuwa mfumo wa kidigitali wa usambazaji wa pembejeo za kilimo utawezesha taarifa na takwimu za mlolongo mzima wa usajili, manunuzi ya mbegu au mbolea, uuzaji kupatikana; yaani ‘traceability’; utazuia pembejeo feki na upandishwaji holela wa bei za pembejeo nchini.  

Aidha , Mhe.Bashe amehitimisha na kusema Serikali iko katika mchakato wa kuandaa sheria na kanuni itakayomlazimu muuzaji wa pembejeo moja kwa moja kwa mkulima kuwa na elimu ya masuala ya kilimo katika ngazi mbalimbali kama Astashahada, Shahada na kadhalika, itakayomuwezesha kutoa elimu sahihi ya matumizi ya pembejeo kwa wakulima katika kuongeza uzalishaji.  Mchakato huo unatarajia kukamilika mwaka 2025.