Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

WIZARA YA KILIMO, UJUMBE KUTOKA DENMARK WAJADILI UWEKEZAJI SEKTA YA KILIMO

Imewekwa: 03 Apr, 2025
WIZARA YA KILIMO, UJUMBE KUTOKA DENMARK WAJADILI UWEKEZAJI SEKTA YA KILIMO

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Dkt. Hussein Mohamed Omar amekutana na ujumbe kutoka Denmark uliongozwa na Balozi wa Denmark nchini Tanzania,  Mhe. Jesper Kammersgaard tarehe 27 Machi 2025, jijini Dodoma.

Ujumbe huo pia umehusisha Makamu wa Rais Shirika la Maendeleo la Denmark anayehusika na ufadhili wa miradi endelevu ya miundombinu, Bi. Tina Kollerup Hansem; Makamu wa Rais wa IFU (Investeringsfonden for Udviklingslande) Shirika linalojihusisha na utoaji wa mitaji kwa makampuni katika nchi zinazoendelea), Bw. Theo Ib Larsen; Mkurugenzi wa Uwekezaji, Bw. Andrew Kuria Githaiga; pamoja na Mwambata Uchumi wa Ubalozi wa Denmark, Bw. Oscar Mkude.

Viongozi hao walizungumza kuhusu kuibua fursa za uwekezaji na ushirikiano wa kifedha katika miradi mbalimbali ya kilimo kupitia mikopo yenye masharti nafuu.  Naibu Katibu Mkuu Dkt. Omar aliueleza ujumbe huo kuwa Serikali imelenga kukuza uchumi wa nchi kufikia uchumi wa kati (second middle income level) ifikapo mwaka 2050 huku kilimo ni miongoni mwa sekta zinazotarajiwa kuchangia mafanikio hayo kupitia mapato.

Dkt. Omar ameainisha maeneo muhimu  yanayohitaji kipaumbele katika uwekezaji baina ya nchi hizo mbili kuwa ni eneo la miundombinu ya uhifadhi wa mazao ikiwemo ya nafaka kwa kuongeza uwezo wa kuhifadhi hadi kufikia tani milioni 3 za mahindi.

Ameainisha eneo lingine ni ujenzi wa vituo vya zana za kilimo ambapo ameeleza kua Serikali inalenga kujenga vituo 200 na kuhakikisha upatikanaji wa vifaa kwa ajili ya usimikaji wa mitambo ya zana za kilimo kwa bei nafuu. pamoja na uongezaji thamani katika mazao ikiwemo korosho.

Eneo lingine ni katika programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) ambapo mashamba ya pamoja ni miongoni mwa maeneo muhimu yanayohitaji uwekezaji katika upande wa miundombinu ya umwagiliaji kama vile kuchimba visima vya umwagiliaji kwa wakulima wadogo.