Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

WIZARA YA KILIMO YAENDELEA NA MABORESHO, RASIMU MKAKATI WA PILI WA TAIFA WA ZANA ZA KILIMO

Imewekwa: 19 Mar, 2025
WIZARA YA KILIMO YAENDELEA NA MABORESHO, RASIMU MKAKATI WA PILI WA TAIFA WA ZANA ZA KILIMO

Wizara ya Kilimo kupitia Idara yake ya Zana za Kilimo na Uongezaji Thamani imefanya kikao cha pamoja kwa kushirikiana na kikosi kazi cha wataalam pamoja na washauri elekezi wa ndani na nje wameandaa Rasimu ya Mkakati wa Pili wa Taifa wa Zana za Kilimo. Kikao kimefanyika tarehe 18 Machi 2025, mkoani Morogoro. 

Kazi ya Kikao hicho ni kuifanyia mapitio, uhariri na maboresho ya kimantiki na kimaudhui rasimu iliyoandaliwa ili hatimaye iwasilishwe kwa ajili ya kuridhiwa na kuidhinishwa kwenye Kikao cha Wadau wa Zana za Kilimo.

Mkakati wa Pili wa Taifa wa Zana za Kilimo unaandaliwa kutokana na Mkakati wa kwanza wa Taifa wa Zana za Kilimo wa mwaka 2006-2016 kufikia ukomo.  Kazi hiyo inatekelezwa chini ya makubaliano yaliyofikiwa mnamo tarehe 10 Mei 2023 baina ya Wizara ya Kilimo na Shirika la Chakula Duniani (FAO) . Mkakati huo una lengo la kuimarisha matumizi, utengenezaji, uendelezaji, uhamasishaji, usimamizi na uratibu endelevu wa teknolojia katika mnyororo wa thamani wa kilimo.

Kikao hicho kimehusisha pia washiriki kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Taasisi na Mashirika ya FAO, SUA, TARI, NIRC, COPRA, CAMARTEC, VETA, ACTN na wadau wa kiufundi wa zana za kilimo kutoka katika kanda saba za kilimo.