Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

ZAO LA PARETO LAZIDI KUPANDA THAMANI

Imewekwa: 11 Nov, 2024
ZAO LA PARETO LAZIDI KUPANDA THAMANI
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Bi. Irene Madeje Mlola amesema zao la Pareto linazidi kupanda thamani kutokana na uzalishaji wake kuongezeka, kuongezeka kwa kipato cha wakulima wanaokadiriwa kuwa takribani 10,000 pamoja na kukuza uchumi wa nchi.  Bi. Mlola amesema hayo wakati alipomwakilisha Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) katika mkutano wa kumi na nne (14) wa wadau wa zao la Pareto uliofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Midland, jijini Dodoma, tarehe 7 Novemba 2024. “Mchango wa fedha za kigeni unaotokana na mauzo ya nje ya zao la Pareto unaendelea kupanda kutoka shilingi billion 15 hadi billion 19 kwa mwaka 2023/2024 ambapo jumla ya wastani wa fedha walizolipwa wakulima wa Pareto zimepanda kutoka shilingi billion 6.2 mpaka billion 13.4 na haya ni mapinduzi makubwa katika sekta ya kilimo”, amesema Bi. Mlola. Bi. Mlola ameeleza kuwa ongezeko hilo linatokana na bei ya zao la Pareto kupanda kutoka wastani wa shilingi 2,600 kwa kilo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 mpaka shilingi 3,700 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kutokana na jitihada za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye kwa kipindi cha miaka mitatu amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha Sekta ya Kilimo inaendelea kupata uwekezaji mkubwa.  Aidha, Bi. Mlola amewahakikishia wakulima kuwa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imejipanga kuwawezesha waendelee kuzalisha Pareto iliyo bora na itaendelea kuwasimamia ili kuongeza uzalishaji bora wa zao hilo. Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Pareto nchini, Bw. Lucas Ayo amesema bei ya zao la Pareto limepanda toka shilingi elfu 3,500 kwa kilo hadi kufikia shilingi elfu 3,700 itakayoanza kutumika tarehe 8 Novemba 2024.  Aidha, Bw. Ayo amebainisha kuwa bei itakuwa na wigo wa kupanda hadi kufikia shilingi elfu 5,000 kwa kilo moja kutokana na ubora wa maua ya zao hilo, huku akiwasisitiza wakulima kuzingatia njia bora za kilimo.  Uzalishaji wa zao la Pareto unatarajiwa kufikia takribani tani 10,000 hadi kufikia mwaka 2030.