ZIARA YA UKAGUZI KITUO MAHIRI CHA ZANA ZA KILIMO ITILIMA SIMIYU

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo, Mifugo na Uvuvi wamefanya ziara katika Kituo Mahiri cha Zana za Kilimo kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, Mkoani Simiyu tarehe 12 Machi 2025.
Akizungumza wakati wa kutoa taarifa ya Mradi huo, Mkurugenzi Wizara ya Kilimo eneo la Zana za Kilimo na Uongezaji Thamani, Mhandisi Anna Mwangamilo, amesema kituo hicho kinatoa huduma za mafunzo ya kuendesha trekta, mafunzo ya kilimo biashara na namna ya kuhifadhi nafaka. Ameongeza kuwa takriban shilingi milioni 200 zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa ofisi na karakana ya kuhifadhia matrekta.
Kuhusu vituo vya zana za kilimo, Mha. Mwangamilo amesema kuwa Wizara imeandaa mwongozo maalumu wa uendeshaji wa vituo hivyo ili kuwezesha na kurahisisha uendeshaji wake kuanzia ngazi ya vijiji na kata ili mkulima apate huduma ya kukodishiwa trekta kwa bei nafuu.
Naye Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Deodatus Mwanyika (Mb) amezitaka Halmashauri zote ambazo miradi hiyo ya kilimo inaendelea kushirikiana na Wizara ya Kilimo ili kurahisisha Serikali kukamilisha miradi hiyo na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Kamati hiyo inaendelea na ziara yake katika mikoa ya Shinyanga na Tabora kukagua miradi mbalimbali ya kilimo huku ikiambatana na waalamu mbalimbali kutoka Wizara ya Kilimo.