Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

ZIARA YA KUTEMBELEA MRADI WA UJENZI BWAWA LA UMWAGILIAJI MEMBE

Imewekwa: 03 Apr, 2025
ZIARA YA KUTEMBELEA MRADI WA UJENZI BWAWA LA UMWAGILIAJI MEMBE

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe. Naghenjwa Kaboyoka (Mb) imetembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa bwawa la umwagiliaji unaofanyika katika Kijiji cha Membe, Wilaya ya Chamwino, mkoani Dodoma tarehe 2 Aprili 2025.

Bwawa la umwagiliaji la Membe linajengwa kwa gharama ya Shilingi Billioni 16.4 ambazo ni fedha kutoka Serikali Kuu kupitia bajeti ya Serikali. Ujenzi huo ulianza mwaka wa fedha 2022/2023 chini ya usimamizi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC). 

Bwawa la Membe litakuwa na uwezo wa kuhifadhi maji mita za ujazo bilioni 12 ambapo yataweza kumwagilia hekta 2,500 za mashamba kwa wakulima zaidi ya 1,500 wa Kata ya Membe na Kata za jirani.

Lengo la kuanzishwa kwa mradi huo ni kuongeza upatikanaji wa maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji wa mazao kama mahindi, mtama, mpunga na mbogamboga ambapo Wakulima watalima misimu miwili kwa mwaka (Masika na Kiangazi).