ZIARA YA WB KUKAGUA UTEKELEZAJI PROGRAMU YA TFSRP

Wajumbe kutoka Benki ya Dunia wakiongozwa na Bi. Frauke Jungbluth ambaye ni Meneja Kilimo na Chakula katika ukanda wa Kusini na Mashariki ya Afrika wa Benki ya Dunia (Practice Manager Agriculture and Food in Southern and Eastern Africa World Bank) wamefanya ziara ya ukaguzi wa utekelezaji wa Programu ya Mifumo Himilivu ya Chakula Tanzania (TFSRP) inayotekelezwa kupitia Wizara ya Kilimo na Taasisi zake, tarehe 12 Machi 2025 jijini Dodoma.
Wamekagua Shamba la Taasisi za Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Hombolo, Skimu ya Umwagiliaji Hombolo, Bwawa la Hombolo (ambalo ni chanzo cha maji ya Skimu ya Umwagiliaji Hombolo), kiwanda cha kuchakata mchuzi wa zabibu kiitwacho Shubi Vintners Limited na Kampuni ya IFL (ITRACOM Fertilizers Limited) jijini Dodoma.
Aidha, wamepata ushuhuda kutoka kwa mjasiliamali na mzalishaji miche ya zabibu, Bw. Fredrick Mwaluko aliyepata mafunzo kutoka TARI aliyewaeleza kuwa amenufaika na mafunzo hayo kwa mwaka 2025 ambapo amezalisha zaidi ya miche 1,000,000 ya zabibu kwa ajili ya kuuza kwa wakulima wa zabibu waliopo maeneo mbalimbali mkoani Dodoma.
Wakiwa katika Kampuni ya Shubi Vintners Limited inayochakata mchuzi wa zabibu na kutengeneza mvinyo inayomilikiwa na Bw. Albert Rutehangwa, wajumbe wa WB walielezwa kuwa uzalishaji wa mchuzi wa zabibu umeongezeka kutoka lita 3,000 kwa mwaka 2021 na kufikia lita 380,000 kwa mwaka 2024 kutokana na ongezeko la uzalishaji wa zabibu unaochangiwa na matokeo ya tafiti zinazofanywa na TARI hivyo kuchangia katika kuongeza uzalishaji kwa wakulima.
Ziara hiyo imehitimishwa kwa kutembelea Kampuni ya ITRACOM Fertilizers Limited (IFL) na kupokea wasilisho kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Dkt. Kenneth Masuki kuhusu kazi zinazotekelezwa na kampuni hiyo.
Wajumbe wa Benki ya Dunia wameambatana na Mratibu wa Programu ya Mifumo Himilivu ya Chakula Tanzania (TFSRP), Bw. Timothy Semuguruka pamoja na wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo na Taasisi zake.